MZIKI WA SIKU HIZI HAUNA UNDERGROUND WALA MKONGWE, WOTE SAWA
Muziki wa siku hizi hauna cha mkongwe wala underground, kama huamini uliza wakongwe flani ambao kwa sasa wanatapa kufa maji. Msanii kujiita underground ni kujidharau mwenyewe. Kinachotofautisha wasanii siku hizi ni bidii na kipaji na sio ukongwe na umaarufu. Kama wasemavyo wahenga kuwa mtaji wa maskini ni nguvu zake, naona pia mtaji wa msanii yoyote ni kipaji na bidii yake.
Zamani kidogo miaka flani ya nyuma kupenya na kuitawala sanaa ilikua rahisi saana kwa sababu ya ufinyu wa ushindani uliokuwepo. Miaka hiyo ambapo sanaa ndio ilikua inajitengenezea jiwe la msingi, msanii alikua anaweza kuimba kitu chochote na watu wakamkubali. Miaka hiyo pia ni wakati ambapo msanii alikua anaweza kutawala chati na wimbo mmoja kwa takriban miaka mitatu akipiga shows na kubaki gumzo kwa midomo ya wengi kwa kipindi kirefu. Hukuhitajika kama msanii kuwekeza pesa nyingi kwa video za ubora kama ilivyo sasa ili ufanye vizuri.Wakati huo pia katika vipindi vingi vya redio hakukua na ushindani mkubwa vile kwa hivyo ilikua ni rahisi wimbo wako kukubalika, kupenya na kutawala vipindi.
Mambo yoote haya yaliruhusu dhana flani itawale katika fikra za wengi. Dhana hii ikiwa ni kuamini kuwa kizuri chatoka tu kwa wale wasanii ambao washatengeneza jina tayari. Dhana hii ilipelekea wasanii wengi wachanga kukanyagiwa na nafasi nyingi kupewa wasanii ambao wamejipatia umaarufu tayari. Hapo ndio nahisi kuwa jina la underground lilipotokea. Kizazi kilichofuata kikawa kizazi cha kuhonga ili kuwezesha mziki wako kuchezwa redioni. Kwa sababu kwa kipindi hicho mziki ulikua bado mchache sokoni, sanaa ilinajisiwa kwa kiwango flani kwani wadau wengi walilazimisha mziki flani sokoni kisa hongo. Wasanii wengi waliweka imani kuwa ili kufanikiwa katika sanaa lazima uhonge Dj au presenter ili waweke kazi zao hewani. Kipindi hiki cha mda kilishuhudia kushuka kwa viwango vya mziki kwani mziki m’bovu ulitawala saana na kulazimishiwa mashabiki huku mziki mzuri ukikanyagiwa. Kwa kiwango flani, wengi wa washikadau ilikua kuuweka mziki wako hewani ilikua ni lazima utoe hela au kama wewe ni msanii wa kike ilikua ni lazma ugawe utam.
Katika kizazi hiki pia, platforms za kujitangaza ni nyingi saana ikiwemo mitandao ya kijamii ambapo msanii anaweza kusambaza na kutangaza kazi zake na aka hit bila msaada wa DJ wala PRESENTER. Kwa mfano, mimi binafsi msanii Mswazi Masauti nilimjua mtandaoni na nikatafuta kazi zake zote baada ya kuskia wimbo wake mmoja nilioupenda na hadi sasa bado namfuatilia. Siku hizi mtu wa kuhongwa sio presenter na Dj tena bali ni shabiki, hivyo basi kila msanii anaumiza kichwa amhonge shabiki na sio kwa pesa bali ni kwa kupitia mziki mzuri. Katika kizazi hiki ukiwa na kipaji ukijiita underground ni kujidharau maana kila siku wasanii wachanga wenye vipaji wanachipuka na kupitia kazi zao nzuri, mashabiki wanawakubali na kupelekea kuwapa wakongwe ushindani sokoni.
Inapendeza kuona kwamba siku hizi wasanii waliochipukia juzi tu wanatumbuiza jukwaa moja na wasanii wakongwe, sio kama curtain raisers bali kama wasanii waliojizolea umaarufu kupitia talanta,ubunifu na bidii. Pongezi ziende kwa wasanii wakongwe kama vile Nyota Ndogo, Ali B, na Susumila miongoni mwa wengine kwa kuhimili ushindani uliopo kwa sasa maana wako wengi ambao wamepotezwa kwenye game kisa ushindani balaa uliopo. Kwa mara ya mwisho, mziki wa siku hizi hauna underground. Talanta,bidii na mpangilio ndio msingi mkubwa wa mafanikio ya msanii.
Comments
Post a Comment